Marehemu Askofu Mkuu Raphael Nding’i Mwana Nzeki wa Kanisa Katoliki na Marehemu Askofu David Gitari wa Kanisa la kianglikana watakumbukwa kama makasisi wa Ujasiri mno.  Walisimama Kidete na kupinga utawala wa kidhalimu wa Rais Moi.

Askofu Ndingi alikua mtu wa Kimo kidogo, ungemtania kama mtu mnyonge ambaye angetishwa na kunyamazishwa, lakini shujaa alitetea haki ya kijamii na kupinga ukandamizi wa wanyonge. Kwenya kilele cha utawala wake,  Rais Moi alitumia Mkuu wa mkoa wa Bonde la Ufa kuchochea uhasama na vita vya jamii eneo la Molo, vita hivi vilisababisha vifo vya karibu watu 2,000. Askofu mjasiri alitembelea eneo la ghasia mle Molo na kwa ujasiri alikemea rais Moi na Mkuu wa Mkoa kwa maovu yao.  Alipinga kukamatwa kwa raia bila kosa, mateso na mauaji ya watu bila kufuata kanuni za sheria. Yeye ni askofu aliyeng’ara kwa ajili ya haki ya kijamii. Ndingi mara nyingi alirejelewa kama “mtu wa kimo kidogo lakini mwenye ujasiri wa Simba”. Alikuwa mtu ambaye hangesita kunguruma dhidi ya ukosefu wa haki wowote katika jamii, bila kujali hadhi ya wale walioueneza.

Kanisa la Anglikana pia lilitupea na maaskofu wa Jasiri watetezi wa Haki za Binadamu, wakiongozwa na viongozi mashuhuri kama marehemu Askofu Dkt. David Gitari, marehemu Askofu Dkt. Henry Okulu, marehemu Askofu Mkuu Manases Kuria, na marehemu Alexander Muge wa Dayosisi ya Eldoret. Kanisa la All Saints Cathedral liko karibu sana na Ikulu, lakini kamwe hakuwahi tembelea Ikulu kujadili ‘Masuala ya Taifa’. Maafisa wa Usalama na jeshi bandia la  Moi ilishinda kuwahangaisha hawa viongozi wa Kanisa lakini walisimama bila shuruti. Mambo yalikua mabaya kiasi kwamba wakati mmoja Gitari akiwa kwake mashinani, Moi aliwatuma vijana wa Kanu kuvamia Askofu Gitari nyumbani mwake huko Kirinyaga. Gitari alitetemeshwa  lakini hakuwai kata tamaa, kwa ujasiri wake aliendelee kukashifu maovu yake rais Moi.

Kutoka Kanisa la Presbyterian tunamkumbuka Mchungaji Timothy Njoya, bado hatujasahau kichapo cha burukenge alichopewa na magaidi wa Moi, Kasisi alishambuliwa kwa inje ya maeneo ya Bunge na kikosi haramu ‘Jeshi La Mzee’. Njoya, pamoja na Wakenya wengine walijitokeza Kupinga Sheria haramu ambayo iliyokua ikijadiliwa bungeni. Njoya amestaafu lakini atasalia kuwa bingwa wa Haki ya Kijamii. Amestaafu kama Kama Shujaa halisi, kamwe Kenya haitamusahau tukiandika kumbu kumbu ya historia ya makasisi shujaa.

Unapoangazia hapo awali unastaabu jinsi hawa ma kasisi walivyo stahimili makali ya Rais Moi. Wakati huo Kenya ilikuwa Nchi ya Chama Kimoja, bila uhuru wa kujieleza, ilikuwa na Kituo kimoja cha Habari kilichokuwa chini ya udhibiti wa serikali, hapakuwa na mitandao ya kijamii kama tuliyo nayo sasa. Hata hivyo, hawa makasisi walisimama ngangari dhidi ya Moi Dikteta. Kwa muhtasari, Kenya wakati huo yaweza kulinganishwa na Korea Kaskazini ya sasa! Siku hizo kua kasisi ilikua ni Wito, sio kama Siku hizi kazi ya kasisi imegeuka kua kama ajira zingine tu.

Katika mfumo wa sasa, tumeshuhudia maovu yakitendeka kutokana na maafisa wa Usalama, utekaji nyara na maafisa wa polisi umerudi, hivi juzi tumeshuhudia vijana waandamanaji kwa amani wakipigwa risasi pasipo hatia, kwenye eneo la bunge hawa wanaharakati walimiminwa risai kama burukenge mchana peupe. Chenye kilitushangaza Taifa nzima ni kwamba Kesho yake Maaskofu wa dhehebu la AIPCA walimtembele Rais Ruto na Kushiriki vipocho pocho ikulu, kana kwamba hakukua tukio lolote la vifo na umwagikaji wa damu! Taifa laomboloza lakini wao washakimbilia kikombe cha chai Ikulu. Hiyo Taswira ilinipiga bumbuazi, hapo ndipo nilimuomba Maulana atufufulie Askofu Ndingi au Gitari angalau kwa siku moja tu wampe rais Ruto ujumbe wa kiunabii.

Tuko katika enzi ya kidijitali sasa, vyombo vya habari viko huru, tuko na uhuru wa kujieleza, tuko na mitandao yote ya kijamii, ajabu ni hatuna kiongozi wa dini hata mmoja mwenye Ujasiri hata robo ya Ndingi, Gitari, au Njoya! Viongozi wa dini wa siku hizi ni madalali walio katika mavazi ya makasisi, wamepanga foleni kuitembele Ikulu kila uchao na kukwachua bahasha za kahawia. Wao bora wameponyoka na kakitu kutoka  ikulu hawajali maovu wanayopitia wanyonge. Hadi sasa bado hawajalaani maovu na machungu tuliyoyashudia, hawajashughulika hata kutembelea majeruhi hospitalini, ama ni kwa sababu hakuna bahasha za kahawia mle hospitalini?

Je, nilisema viongozi wetu wa dini ni madalali? Hapa Kenya, mukijikuta katika mashindano ya kisiasa, ndio uweze kumtisha mpinzani wako, si tumeshuhudia wanasiasa wakikodisha Maaskofu au wachungaji  waweke upako na kukutabiria aliyewaita.  Hatimaye sherehe ya ‘Roho wa Bwana Amenena’ inahitimishwa na bahasha za kahawia. Hawa siku hizi waongozwa na Roho Mtaka Kitu!

Kenya itakukosa Askofu Ndingi na Askofu Gitari, ni sasa tumetambua kuwa mlikuwa na wito na Ujasiri. Tunajua Rais Moi aliwashawishi na bahasha za kahawia mukakana, hata vipocho muliandaliwa Ikulu  lakini mulikataa kimaso maso. Nyinyi ni kama  Musa, mulikana anasa ya Ikulu ya Farao, badala yake mkachagua kusimama na dhiki za Waisraeli.

Endeleeni Kupumzika kwa Amani! Hawa Makasisi  wengine ni SUMU BARIDI kwa Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)